TANESCO yamkamata ‘kishoka’ aliyemuunganishia mteja umeme kwa mita ya zamani

Fundi ‘kishoka’ amekamatwa Kahama mkoani Shinyanga baada ya kudaiwa kumuunganishia mteja umeme kwa kutumia mita ya zamani isiyokuwa na rimoti, huku akidaiwa kushirikiana na baadhi ya mafundi wa TANESCO.

Fundi huyo, Jamari Julius (30), mkazi wa Mhungula, Manispaa ya Kahama, amekamatwa na TANESCO kwa kushirikiana na wananchi baada ya mteja, Hamza Yahya (53), kufika Ofisi za TANESCO Kahama kutoa taarifa kuhusu mita aliyofungiwa.

Ofisa Usalama wa Miundombinu wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Frank Njavike, amesema taarifa hiyo ilipokelewa Septemba 23, saa 3:30 asubuhi, baada ya mteja kufika ofisini kulalamikia kuunganishiwa huduma kwa kutumia mita isiyokuwa na rimoti.

Amesema wataalamu wa TANESCO walifika katika eneo hilo na kukagua mita iliyokuwa imefungwa ukutani, ambapo walibaini kuwa ni mita ya zamani.

Njavike amesema kukamatwa kwa fundi huyo kumewezekana kutokana na ushirikiano kati ya TANESCO na wananchi, ambao wamekuwa wakitoa taarifa kuhusu viashiria vya hujuma dhidi ya miundombinu ya umeme au ukiukwaji wa taratibu.

Akieleza alichokiona, Yahya amesema wakati mafundi walipofika kumfungia huduma ya umeme hakuwepo nyumbani, hivyo kazi hiyo ilisimamiwa na kijana wake.

Amesema baadaye kijana huyo alimweleza kuwa mita iliyofungwa haikuwa na rimoti na ilikuwa imewekwa ukutani, hali iliyomfanya awasiliane na fundi huyo kutaka maelezo kuhusu mahali rimoti ilipo na namna angeitumia baada ya umeme wa mita kuisha.

Yahya amesema majibu aliyoyapata hayakumridhisha, hivyo akaamua kufika Ofisi za TANESCO Kahama kutoa taarifa.

Baada ya kukamatwa, Jamari amekiri kuwa alishirikiana na baadhi ya mafundi wa TANESCO Ofisi ya Kahama kumuunganishia mteja huyo huduma ya umeme, na kwamba walilipwa Sh450,000, ambapo yeye alipata Sh100,000.

TANESCO inaendelea kuchunguza mazingira ya tukio hilo na hatua zaidi kuchukuliwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii