Serikali ya Kenya imeteketeza rasmi shehena kubwa ya dawa za kulevya aina ya methamphetamine yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.2 za Kenya, ikiwa ni pigo kubwa kwa mitandao ya kimataifa ya walanguzi. Zoezi hilo lilifanyika katika kiwanda cha saruji cha Bamburi mjini Mombasa chini ya usimamizi wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ambapo kilo 1,024 za dawa hizo ziliharibiwa kwa kutumia matanuru ya joto kali.Shehena hiyo ilinaswa na Jeshi la Wanamaji la Kenya mnamo Oktoba 2025 umbali wa kilomita 630 kwenye Bahari ya Hindi ndani ya jahazi ambalo halikuwa na usajili, na kusababisha ukamatwaji wa raia sita wa Iran wanaokabiliwa na mashtaka ya ulanguzi. Waziri Murkomen alionya kuwa serikali itaongeza msako na kutaifisha mali zote zinazotokana na biashara hiyo ili kuzuia nchi hiyo kutumika kama njia ya kupitishia mihadarati.