Mutafungwa amesema ajali hiyo imehusisha pikipiki yenye namba za usajili MC.647 DCM aina ya Skymark, iliyokuwa ikiendeshwa na Stiven Muhina.
“Dereva huyo akiwa njiani akitokea Malya Kati kuelekea eneo la Mjini A, alipoteza mwelekeo wa pikipiki na kwenda kugonga mti uliokuwa kando ya barabara, hali iliyosababisha kifo chake papo hapo,” amesema Mutafungwa.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi pamoja na viashiria vya ulevi, kufuatia taarifa za marehemu kuonekana akinywa pombe kabla ya safari.
“Ni wazi kwamba madhara ya ajali hiyo yaliongezeka kutokana na marehemu kutovaa kofia ngumu (helmet) wakati wa uendeshaji wa chombo hicho cha moto,” ameeleza Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Mutafungwa, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa ajili ya taratibu za kisheria na uchunguzi wa kitaalam kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Itakumbukwa kuwa, siku chache zilizopita Mwenyekiti huyo alisaidia kutatua changamoto ya maji baada ya kuwasilisha kero ya maji kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda katika kata ya Malya.
Ambapo, jana akiwa kwenye muendelezo wa ziara yake wilayani Ukerewe, Waziri Makonda alieleza kusikitishwa kwake na kifo hicho.
Kutokana na ajali hiyo, Mutafungwa ametoa wito kwa madereva wote, hasa wa pikipiki, kuacha tabia ya kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, kutembea kwa mwendokasi na kupuuzia matumizi ya kofia ngumu.
“Hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa bila muhali dhidi ya yeyote atakayebainika kuvunja sheria za usalama barabarani,” amesema.