Mazishi ya Alute Mughwai Kusubiri Hukumu ya Kesi ya Lissu

Familia ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, imeamua kusogeza mbele mazishi ya kaka yao, Wakili Alute Mughwai Lissu, hadi baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili ndugu yao huyo, inayotarajiwa kusomwa Novemba 6, 2026, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Vincent Lissu Mughwai amesema familia imepanga kufanya mazishi ya marehemu Alute mkoani Singida, lakini tarehe rasmi itatangazwa baada ya hukumu ya kesi ya Tundu Lissu kutolewa.

Amesema uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kutoa nafasi kwa wanafamilia kushiriki katika usomaji wa hukumu ya Tundu Lissu na baadaye kushiriki katika shughuli za mazishi ya kaka yao.

Dkt. Vincent ameeleza kuwa familia inaamini Tundu Lissu hana hatia na inatarajia ataachiwa huru baada ya hukumu hiyo, ili aweze kushiriki katika mazishi ya kaka yake.

Aidha, amebainisha kuwa marehemu Alute alikuwa akiugua kwa muda mrefu na aliwahi kulazwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha, kabla ya hali yake kuzidi kuwa mbaya kuanzia siku za hivi karibuni na hatimaye kufariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 1, 2026.

Marehemu Alute amefariki akiwa na uhusiano wa karibu wa kindugu na Tundu Lissu, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Ikumbukwe kuwa mahakama hiyo imepanga kutoa hukumu ya kesi hiyo Novemba 6, 2026, baada ya pande zote mbili kukamilisha mawasilisho yao ya mwisho.

Hadi sasa, familia haijatangaza tarehe rasmi ya mazishi ya Wakili Alute Mughwai Lissu, ikisubiri kwanza hatua ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii