Kanye West Akumbana na Pigo Russia

Matamasha mawili ya mwanamuziki wa Marekani Kanye West, anayejulikana pia kama Ye, yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini Russia mwezi Oktoba yamefutwa.

Kwa mujibu wa waandaaji wa matamasha hayo, Say Agency, West alitarajiwa kutumbuiza katika jiji la St Petersburg. Hata hivyo, mpango huo uliingia kwenye sintofahamu baada ya ukumbi uliopangwa kutumika kudai kuwa haukuwa umesaini mkataba na kampuni iliyokuwa ikiandaa matamasha hayo.

Matamasha hayo yalitangazwa kwa mara ya kwanza katikati ya Agosti, lakini wiki moja baadaye ukumbi uliokuwa umetajwa kuwa mwenyeji ulisema haukuwa na mkataba na waandaaji.

Tangu wakati huo, hatma ya matamasha hayo haikuwa wazi, huku waandaaji wakishindwa kutoa uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu kama yangefanyika.

Siku ya Jumatano, Say Agency ilitangaza kupitia Telegram kwamba matamasha hayo hayatafanyika katika tarehe zilizopangwa, huku ikiahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu mustakabali wa mradi huo.

Kufutwa kwa matamasha hayo kunakuja wakati West akikabiliwa na changamoto mbalimbali katika shughuli zake za muziki barani Ulaya.

Mwanamuziki huyo amewahi kukumbana na kufutwa kwa baadhi ya matamasha na kuzuiwa kutumbuiza katika baadhi ya nchi za Ulaya kufuatia kauli zake za chuki dhidi ya Wayahudi, ambazo kwa nyakati mbalimbali zilihusisha kumsifu Adolf Hitler na kutumia alama zinazohusishwa na utawala wa Nazi.

West aliomba radhi mwezi Januari kuhusu baadhi ya kauli hizo, akizihusisha na jeraha la ubongo ambalo hakujua kuhusu awali pamoja na ugonjwa wa bipolar ambao alisema haukuwa umetibiwa.

Iwapo yangefanyika, matamasha hayo yangemfanya West kuwa miongoni mwa wasanii wakubwa wa kimataifa kutumbuiza nchini Russia tangu Moscow ilipoanzisha uvamizi kamili wa Ukraine mwaka 2022.

Mpango huo pia ulikumbana na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wanablogu wa kijeshi nchini Russia wanaounga mkono vita, ambao walihoji uamuzi wa kumwalika msanii kutoka Marekani wakati Washington ikiendelea kuisaidia Ukraine kijeshi na kifedha.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, pia alikosoa mpango huo, akisema ulikuwa haukubaliki na akirejea kile alichokiita “kutukuzwa” kwa Hitler na West.

Kwa sasa, waandaaji wamesema watatoa taarifa nyingine kuhusu hali ya mradi huo na mipango yao ya baadaye.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii