LAKE VICTORIA MARATHON KUWAGUSA WATOTO NJITI

Mashindano ya riadha yanayofahamika kama Lake Victoria Marathon yanatarajiwa kufanyika Novemba 15, 2026, jijini Mwanza, yakilenga kuhamasisha utunzaji wa Ziwa Victoria, kuimarisha afya za wananchi na kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya watoto njiti katika Kanda ya Ziwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 10, 2026, jijini Mwanza, Mratibu wa mashindano hayo, Hilda Viggo, amesema msimu wa sita umejikita katika kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa Ziwa Victoria kwa lengo la kulinda mazingira na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka ziwa hilo.

“Tangu kuanzishwa kwa mashindano haya, tumekuwa tukisisitiza umuhimu wa kutunza mazingira, jambo linaloonekana pia katika kauli mbiu yetu ya ‘Preserve and Conserve’,” amesema Hilda, akibainisha kuwa kauli mbiu ya msimu huu ni “Kimbia Kiafya, Kimbia na Ziwa Victoria, Kimbia Kiviwango.”

Hilda amesema mashindano hayo pia yanalenga kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili.

“Mwaka huu tunalenga kuchangia mahitaji ya watoto wasiopungua 4000 ambao hupoteza maisha kila mwaka kutokana changamoto za kiafya zinazowakabili watoto wanaozaliwa kabla ya wakati,” amesema.

Amesema mashindano hayo yatakuwa na vipengele vinne vya mbio, ambavyo ni kilomita 2.5 zinazojulikana kama Kids Challenge, kilomita tano, kilomita 10 zinazojulikana kama Corporate Run, pamoja na kilomita 21 za Half Marathon.

Ameongeza kuwa mashindano ya mwaka jana yalishirikisha zaidi ya watu 2,800, huku mwaka huu waandaaji wakilenga kufikisha washiriki wasiopungua 3,000 ili kuongeza ushiriki wa jamii na mchango kwa watoto njiti.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuanzia na kumalizikia katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza, Edwin Emmanuel Ngonyani, amesema chama hicho kimejipanga kuhamasisha wanariadha na wananchi kushiriki kwa wingi katika mashindano hayo.

“Tumeguswa na mpango wa mashindano haya wa kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati. Tunawahimiza wananchi kujisajili mapema ili kuongeza idadi ya washiriki na kuhakikisha mashindano yanafanikiwa,” amesema Ngonyani.

Naye, Meneja Biashara wa Mixx by Yas, Charles Elisante, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na waandaaji pamoja na Serikali katika kuhakikisha watoto njiti wanapata msaada unaohitajika.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo imeboresha wigo wa mawasiliano kupitia huduma zake, huku ikitarajia kupata washiriki wengi kutoka Mwanza na nchi jirani.

Mashindano hayo yameandaliwa na Lake Victoria Marathon kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo Mixx by Yas na SBA Security.

Imeandaliwa na: Martin Mbilinyi

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii