Watu wanne wamefariki dunia na wengine 11 kujeruhiwa baada ya ukuta uliokuwa ukijengwa kuporomoka na kuwafukia wafanyakazi katika eneo la Riverside Drive, jijini Nairobi, Kenya.
Vyombo vya habari vya ndani vimebainisha kuwa tukio hilo limetokea leo asubuhi karibu na jengo la Grand Residence wakati wafanyakazi walipokuwa wakifika kuanza majukumu yao ya kila siku, ambako ukuta huo ulisadikiwa kuporomoka ghafla na kuwafukia baadhi yao.
Kwa mujibu wa chanzo cha kiusalama kilichokuwepo eneo la tukio, wafanyakazi wa vibarua 33 walikuwa karibu na ukuta huo wakati ulipoporomoka.
Pia vyanzo vilieleza kuwa timu za uokoaji, wahudumu wa dharura na viongozi wa mamlaka za eneo hilo walifika haraka kuendesha zoezi la uokoaji na kuwasaidia walioathirika.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa wafanyakazi 22 walikuwa wamepatikana na kutambuliwa, huku 11 waliojeruhiwa wakikimbizwa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi kwa matibabu.
Polisi wamefunga eneo la tukio wakati shughuli za uokoaji zikiendelea ili kubaini iwapo kuna watu wengine walionasa chini ya vifusi.
Uchunguzi unatarajiwa kubaini chanzo cha kuporomoka kwa ukuta huo na iwapo ujenzi ulizingatia viwango na taratibu za usalama zinazotakiwa.
Tukio hilo limetokea siku moja baada ya jengo jingine kuporomoka katika Barabara ya Mombasa, na kusababisha vifo vya watu sita, hali iliyozua upya wasiwasi kuhusu usalama wa shughuli za ujenzi jijini Nairobi.