Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha ACT Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Luhaga Mpina, ameitaka Serikali kuhakikisha kunakuwepo na msuluhishi huru atakayekubalika na pande zote kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya maridhiano nchini.
Mpina amesema mchakato huo unapaswa kujengwa katika misingi ya ukweli, haki na uwajibikaji, akieleza kuwa si sahihi kwa upande unaohusika katika mgogoro kusimamia wenyewe mchakato wa kuutatua bila chombo huru cha usuluhishi.
Akizungumza na waandishi wa habari, amesema taasisi za dini, asasi za kiraia na vyama vya siasa vinapaswa kusubiri hadi misingi ya maridhiano itakapowekwa wazi kabla ya kupendekeza wawakilishi watakaoshiriki katika Tume ya Maridhiano inayotarajiwa kuundwa na Serikali.
Ametoa mfano wa Afrika Kusini na Kenya, akisema uzoefu wa nchi hizo unaonesha umuhimu wa kuendesha michakato ya maridhiano kwa kuzingatia haki, uwazi na ushiriki wa pande zote zinazohusika.
Katika hatua nyingine, Mpina ametangaza kufungua mashauri manne katika Mahakama Kuu ya Tanzania, akisema hatua hiyo inalenga kulinda Katiba, rasilimali za umma na uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali.
Amesema shauri la kwanza linapinga kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi, huku akiomba Mahakama ibatilishe uamuzi huo na kutambua uhalali wa nafasi yake kwa mujibu wa hoja alizowasilisha.
Shauri la pili linahusu utoaji wa misamaha ya kodi kupitia mikataba ya msingi ya uwekezaji (Framework Agreements). Mpina amesema anaiomba Mahakama kufuta vifungu vya Sheria ya Fedha ya mwaka 2026 anavyodai vinaweza kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
Amesema shauri la tatu linahusu mikataba ya rasilimali za nchi, ambapo anaiomba Mahakama kuiamuru Serikali kuweka wazi mikataba yote iliyoingiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali hizo.
Kwa mujibu wa Mpina, shauri la nne linahusu mikopo ya Serikali, akitaka kuwekwa wazi orodha ya mikopo iliyoingia nchini na matumizi yake kuanzia Machi 2021 hadi Desemba 2025 ili wananchi wafahamu namna fedha hizo zilivyotumika.
Aidha, amevitaka vyama vya upinzani kuimarisha umoja na kuunganisha nguvu katika kutekeleza majukumu yao ya kisiasa, akisema migogoro ya ndani na kutokuelewana kunadhoofisha vyama hivyo.
Amesisitiza kuwa maridhiano yenye mafanikio yanahitaji utashi wa kisiasa, uwazi na ushiriki wa msuluhishi asiyeegemea upande wowote.