Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Samia Suluhu Hassan ameridhia kusamehewa riba ya kodi ya pango la ardhi
kwa wadaiwa sugu kwa masharti kwamba wadaiwa hao wawe wamelipa madeni
ya msingi ndani ya miezi sita kuanzia mwezi julai hadi desemba 2022.
Hayo
yamebainishwa tarehe 12 Julai 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika mkutano na wananchi wa
kijiji cha Nyachoka wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa zoezi la
kukabidhi hati miliki za kimila.
Jumla ya hatimiliki za kimila
6,155 zimekamilika na kutolewa kwa wananchi wa vijiji 22 katika wilaya
ya Serengeti ambapo hati 1621 sawa na asilimia 26 zimekamilishwa kwa
ajili ya akina mama na hatimiliki 1519 sawa na asilomia 25 ni za
umiliki pacha kati ya wanaume na wanawake.
Dkt Mabula alisema
yeye pamoja na Waziri wa Fedha ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusamehe
watakutana na kupanga namna bora ya kutekeleza msamaha huo.
“Najua
kuna wengi wanadaiwa madeni ya muda mrefu kwa hiyo kumetokea msamaha
kuanzia mwezi julai mpaka desemba mwaka huu, watakaoweza kulipa ndani ya
miezi hii sita, wale ambao madeni yao yana miaka mitano kurudi nyuma
watalipa bila ile tozo ya riba” alisema Dkta Mabula.
” Mhe mama
samia ameridhia kupitia waziri wa fedha kwa kushirikiana na waziri wa
ardhi waweke utaratibu mzuri wa ninyi kuondolewa tozo ile na msamaha ni
wa miezi sita tu kama una ndugu mpigie simu mwambie serikali ya awamu ya
sita chini ya mama samia imetoa msamaha kwa wadiwa sugu ili watoke
katika jina baya la wadaiwa sugu kwenda kulipa madeni bila riba” alisema
Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, mmiliki wa ardhi
atakayeshindwa kulipa madeni yake katika kipindi cha miezi hiyo sita
basi atadaiwa madeni yake pamoja na riba na akishindwa kufanya hivyo
atafikishwa kwenye vyombo vya sheria ambako huko uamuzi wake ni kulipa
ama kunyang’anywa ardhi anayoimiliki.
Akigeukia zoezi la utoaji
hatimiliki za kimila Dkt Mabula alisema, hatua ya kumilikishwa ardhi kwa
nyaraka kuna faida kubwa katika maisha ya kila siku na kutaja baadhi ya
faida hizo kuwa ni pamoja na usalama wa ardhi, uhakika wa milki,
kupunguza migogoro pamoja na nyaraka hiyo kutumika kama dhamana.
Zaidi
ya wananchi 6000 katika vijiji 22 wamepangiwa matumizi bora ya ardhi
katika maneo yao na kuwekewa mipaka ya kudumu ili kuepuka migogoro ya
mipaka kwenye ardhi zao
Serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya
Serengeti, Shirika la Hifadhi la Taifa Serengeti (SENAPA) na Shirika la
Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo
ya Ujerumani (KFW) kupitia mradi wa utunzaji na uendelezaji wa Ikolojia
ya Serengeti waliingia makubaliano ya pamoja kwa ajili ya kuwezesha
uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ya vijjji vinavyopakana na
maeneo yaliyohifadhiwa yanayounda ikolojia ya serengeti inayojumuisha
hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Madhumuni ya mradi huo ni
pamoja na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya vijiji na eneo
la hifadjhi , kutatua migogoro ya mipaka kati ya maneo ya kiutawala
pamona na kutoa elimu ya uhifadhi na sheria mbalimbambalj zinazosimamia
mipango ya matumiZi ya ardhi nchini.