Baraza la Umoja wa Ulaya linalowakilisha nchi wanachama 27 limeidhinisha kuipa Ukraine msaada wa fedha wa Euro bilioni moja wakati ambapo Urusi inazidisha uvamizi nchini humo. Mawaziri wa fedha wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya wamesema fedha hizo zitatolewa kama mkopo kuongezea mkopo mwingine wa Euro bilioni 1.2 uliotolewa kwa Ukraine mnamo mwezi Februari. Waziri Mkuu wa Ukraine pia amethibitisha kuwa nchi yake imepokea msaada wa dola bilioni 1.7 kutoka Marekani. Fedha hizo kutoka Marekani zitatumika kwa ajili ya mishahara ya wahudumu wa afya na kwa ajili ya kugharamia huduma nyingine muhimu. Ukraine inakadiria kiasi cha Euro bilioni 750 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu baada ya vita.