Rais Joe Biden ajitetea juu ya kufanya ziara Saudi Arabia

Rais wa Marekani Joe Biden ametetea ziara anayotarajia kufanya nchini Saudi Arabia mnamo wiki hii. Biden amesema katika makala aliyoandika kwenye gazeti la Washington Post kwamba sera yake ya nje imelifanya eneo la Mashariki ya Kati liwe imara na salama zaidi kulinganisha na hali iliyvokuwa wakati wa utawala wa rais wa hapo awali Donald Trump. Biden ameeleza kuwa ziara yake pia inahusiana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na pia mashindano na China ambapo amesema Saudi Arabia inaweza kutoa mchango muhimu. Kiongozi huyo wa Marekani amesisitiza kuwa msimamo wake juu ya maswala ya haki za binadamu unaeleweka wazi, na ni wa kimsingi. Mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman anatuhumiwa kuhusika na kuuliwa kwa mwandishi habari Jamal Khashoggi mnamo mwaka 2018 nchini Uturuki. Kashoggi alikuwa mwandishi wa gazeti la Washington Post.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii