Burundi kuwatuma wanajeshi wake katika Mji wa Bukavu nchini DRC

Nchi ya Burundi, imetuma wanajeshi wake katika eneo la Gatumba kwenye mpaka wa DRC, ambapo wanatarajiwa kutumwa katika Mji wa Bukavu, Mji Mkuu wa Kivu Kusini.

Tangu mwaka wa 2023 mwezi Septemba, Burundi ilitia saini makubaliano ya kijeshi na DRC, hatua ambayo imeifanya Bujumbura kujihusisha moja kwa moja na mzozo unaoendelea mashariki ya Kongo.

Burundi imewatuma wanajeshi wake (FDNB) Elfu 10 katka nchi jirani ya DRC kuisaidia katika vita vyake dhidi ya waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Vyanzo vya kiusalama vinasema kufikia sasa nchi hiyo imewatuma karibia wanajeshi Elfu nane hadi Elfu 12 kwenda nchini DRC.

Inaelezwa kwamba vitengo 16 vya wanajeshi wa Burundi vipo nchini DRC ambapo vitano vipo kwa miji ya Fizi na Uvira ambapo vinapambana na waasi wa RED-Tabara wenye asili ya Burundi.

Wanajeshi hao wa Burundi wanatarajiwa kuweka kambi yao katika Mji wa Bukavu kujaribu kuwazuia waasi wa M23 kuingia kwenye eneo hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii