Milioni 98 kuanzisha ujenzi Kituo cha Mabasi Rorya

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amesema Serikali imeweka mikakati dhabiti kwaajili ya kujenga kituo cha mabasi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambapo Milioni 98 zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo kwa hatua za awali.
Dkt. Dugange ameyasema hayo leo Aprili 9, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rorya, Jafari Chege aliyehoji ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya muda mrefu ya kuwajengea wananchi wa Rorya stendi yao.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge huyo aliyehoji, kuna mpango gani wa ujenzi wa stendi Wilayani Rorya ili kuongeza mapato ya Halmashauri, Dkt. Dugange amesema Serikali inatambua umuhimu wa Wananchi wa Rorya kuwa na Stendi ya Mabasi kwa lengo la kuongeza mapato ya Halmashauri na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.

"Kwa sababu hiyo, Serikali kupitia Halmashauri imetenga eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 10 katika Kijiji cha Mika na Nyasoko kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya Wilaya ya Rorya,” amesema.
“Kwa kuanza, Halmashauri kupitia mapato ya ndani imetumia shilingi milioni 98 kujenga stendi ya muda katika Kijiji cha Mika ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya stendi na kuongeza mapato ya halmashauri ya Rorya,” alibainisha Naibu Waziri.
Pia ameongeza kuwa Halmashauri ya Rorya imefanya mazungumzo ya awali na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) chini ya Wizara ya Fedha ili kuweza kutekeleza mradi huo wa Kimakakati.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii