RAIS WA NAMIBIA AWASILI UKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah amewasili nchini jana May 20  2025 kwa ajili ya kuanza ziara  yake rasmi ya siku mbili kuanzia May 20 hadi May 21, 2025.

Ziara hiyo ya kwanza kwa Nandi-Ndaitwah kufanyika hapa nchini tangu kuingia kwake madarakani mwezi March 2025 kutokana na kufuatia kwa mwaliko uliotorewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam, Dkt. Nandi-Ndaitwah amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Akiwa nchini pamoja na mambo mengine Dkt. Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo ya faragha na Mwenyeji wake Rais Samia  yatakayofuatana na mazungumzo rasmi ya kujadili namna ya kukuza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Kadhalika Viongozi hao kwa pamoja  watazungumza na Waandishi wa Habari ili kuelezea makubaliano waliyofikia katika mazungumzo yao kabla ya kushiriki dhifa ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima ya Dkt. Nandi-Ndaitwah.

Akiendelea na ziara yake nchini Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah May 21, 2025 anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kutembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kilichopo Dar es salaam.

Ikumbukwe kuwa tanzania na Namibia zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na Waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sam Nujoma kupitia mikataba mbalimbali ya uwili na masuala yote yanayohusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii