KATIBU AMCOS AHUKUMIWA MIAKA 20 JERA

Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemuhukumu kwenda jela miaka 20 Katibu wa Chama Cha Ushirika cha Msingi (Amcos) Kijiji cha Gula mkazi wa wilayani hiyo Masanja Mboje (36) baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya rushwa na uhujumu uchumi.

Mboje pia ameamriwa kurejesha Sh3.3 milioni  ambazo alizifanyia ubadhirifu ikizingatiwa kuwa kati ya Sh3.5 milioni  alikuwa tayari amerejesha Sh200,000.

Hukumu hiyo ilitolewa Jumanne Mei 20, 2025 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Aziz Hamis baada ya mshtakiwa kukiri makosa yake kulingana na hati ya mashitaka katika kesi ya uhujumu uchumi.

Katibu huyo kwa mujibu wa hati ya mashitaka alifikishwa mahakamani hapo Januari 3,2025 akishtakiwa kwa makosa wawili ufujaji na ubadhilifu wa fedha kinyume na Kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura no 329 Marejeo ya Mwaka 2019 vilivyosomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza pamoja na vifungu vya 57(1)na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa sura 200 Marejeo ya mwaka 2022.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Maswa Bahati Madoshi alieleza Mahakama hapo kuwa mshitakiwa akiwa Katibu wa Amcos ya Gula na mtu pekee aliyekabidhiwa mamlaka ya kununua pamba kutoka kwa wakulima alikuwa akitumia fedha hizo kwa matumizi yake binafsi Sh3.5 milioni ambazo alipaswa kumlipa Edward Mathias baada ya kupeleka pamba yake yenye uzito wa kilo 2,268.

Ameendelea kuieleza Mahakama kuwa kwa kufanya hivyo alikiuka mwongozo namba 1 wa msimu wa mwaka 2024/2025 kuhusu mfumo wa usimamizi na uuzaji wa pamba uliotolewa kwa Sheria ya tasnia ya pamba namba 2 ya mwaka 2011 unaotolewa na Bodi ya Pamba Tanzania.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii