JKT YAHAMASISHA VIJANA KUJIUNGA NA MAFUNZO

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele amewatoa hofu wazazi kuhusu mafunzo yatolewayo na JKT, kwani wanapatiwa vijana wao kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza leo Mei 21, 2025 katika Kikosi cha Jeshi cha Makutupora JKT mkoani Dodoma, Meja Jenerali Mabele amesema mafunzo yanayotolewa na jeshi hilo hayaambatani na mateso wala manyanyaso  hivyo wazazi wasisite kuwaruhusu na kuhamasisha watoto wao kuripoti katika kambi za jeshi pale wanapoitwa baada ya kuhitimu kidato cha sita.

“Sisi kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ni kwamba tunamuongoza kijana aendane na maadili ya Kitanzania, kwa hiyo tunatarajia kuwapokea vijana kwa mujibu wa sheria ambao kwa sasa hivi tunachukua wa kidato cha sita, sio wote kabisa lakini tuna kigezo ambacho tunatumia ili tuweze kupata angalau vijana kwa uwiano sahihi wa wasichana na wavulana ili wahudhurie mafunzo hayo,”

“Wazazi wana mashaka na watoto wao, naomba niwahakikishie wazazi kwamba hawa vijana wanaokuja hapa wanakuja kulelewa hawaji kuteswa, hawaji kunyanyaswa. Tunawaelekeza, ndio maana tunasema tunawapa Basic Military Training yani tunawapa zile values za Taifa letu zinatakiwa kuwa vipi lakini vile vile tunawafundisha namna ya kujitegemea”. amesema Meja Jenerali Rajabu Mabele

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii