WANANCHI WILAYANI RORYA KUNUFAIKA NA KOZI FUPI ZA UJUZI WA UVUVI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) imezindua Mafunzo ya Kozi fupi za Uvuvi na kuboresha Miundombinu ya Kampasi hiyo ya Gabimori ikiwa ni pamoja na kujenga Madarasa mawili kwa ajili ya Mafunzo na Miundombinu ya msingi wa vitotoleshea  Vifaranga vya Samaki, Vizimba viwili vya kufugia Samaki, Recirculating Aquaculture System (RAS), na Birika la kunyweshea Mifugo.

Alizungumza hayo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede Mei 20, 2025 wilayani Rorya mkoa wa Mara wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi ya FETA Gabimori  na kusema kuwa FETA imeanzisha rasmi Mafunzo ya Kozi fupi  ili wananchi waweze kujifunza jinsi ya kufuga Samaki kwa njia ya Vizimba na mabwawa.

“Leo tunazindua Programu za Mafunzo ya Kozi fupi hapa FETA Gabimori ili ianze kuwanufaisha wanajamii wanaozunguka eneo hili na wengine kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo nje na Mkoa wa Mara ili waweze kujifunza shughuli za Uvuvi na ukuzaji viumbe maji. ameseama Dkt. Mhede

Dkt. Mhede amesema kuwa Vifaranga vilivyopandikiza ni 35,000, ambapo vifaranga 4,000 vimepandikizwa kwenye vizimba viwili vya mafunzo ya vitendo na kwenye bwawa (lambo) vimepandikizwa vifaranga 31,000 vyenye gramu kumi mpaka kumi na tano katika bwawa lenye ujazo wa maji lita milioni kumi.

Vilevile Dkt. Mhede amefafanua kuwa vifaranga  vya samaki vitakuwa vinazalishwa FETA Kampasi ya Gabimori ili wale watakaokuwa wameanzisha vikundi vya miradi ya Ufugaji samaki kwa njia ya vizimba waweze kupata vifaranga kwa gharama nafuu.

Aidha Dkt. Mhede amebainisha kuwa FETA Gabimori kuna mradi unganishi ambao unahudumia pia Mifugo ambapo kuna Birika la kunyweshea Mifugo na Miundombinu ya Uvuvi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt. Semvua Mzighani amesema kuwa miundombinu ambayo imejengwa itasaidia Kampasi ya Gabimori kutoa Mafunzo ya Muda mfupi na ya muda mrefu (pale ambapo miundombinu yote ya chuo itakuwa imekamilika).

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii