Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi Mei 21, 2025, ameshuhudia hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa Mkopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya CRDB wenye thamani ya Shilingi Bilioni 240, sawa na Euro milioni 79.
Mkataba huo ulilanga kugharamia ujenzi wa shule 23 za kisasa za ghorofa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ukiwa ni mkopo mkubwa wa kwanza kupatikana kutoka nje ya nchi bila dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu Mapinduzi ya mwaka 1964.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Zanzibar Benki ya CRDB iliwakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu Ndg. Abdulmajid Nsekela huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwakilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akil.
Akizungumza katika hafla hiyo Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa mkopo huo ni matokeo ya ushirikiano wa kimataifa kati ya Benki ya CRDB na Benki ya Udachi (Deutsche Bank) chini ya dhamana ya Bima ya CESCE kutoka Uhispania.
Mbali na ujenzi wa shule mkopo huo utagharamia pia ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara, maktaba, TEHAMA, na samani za walimu na wanafunzi.
Aidha, Rais Mwinyi alieleza kuwa Zanzibar imejipanga kutekeleza miradi mingine mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, uboreshaji wa Uwanja wa Ndege Pemba, ujenzi wa barabara za Chake Chake–Mkoani na Kisauni–Fumba, ujenzi wa Uwanja wa Soka wa kisasa kwa ajili ya AFCON 2027, Hospitali za Mikoa na Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Saratani.