KAULI YA SERIKALI KUHUSU WANAFUNZI KUSIMAMA KWENYE MAGARI YA USAFIRI

Mbunge wa Viti Maalumu Latifa Juakali amesema baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi hupanda mabasi ya shule bila nafasi ya kuketi kwa mwaka mzima hali inayowaathiri kushuka kimaendeleo na kimaadili.

Akizungumza bungeni leo, Alhamisi Mei 22, 2025, Latifa ameitaka Serikali kutoa kauli kuhusu shule zinazokiuka haki hiyo na kupendekeza kuwepo kwa wasimamizi wa kike na kiume ndani ya mabasi ya shule. Pia amehoji haja ya kuwepo kwa walimu wa maadili mashuleni.

Akijibu, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-Tamisemi, Zainab Katimba amesema Serikali imeshaelekeza kuwepo kwa wasimamizi wa jinsia zote katika mabasi ili kuhakikisha usalama wa watoto na amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa walimu na wadau wengine kuhusu ulinzi wa wanafunzi.

Aidha ametaja kampeni dhidi ya ukatili wa kijinsia, mafunzo kwa walimu wa ushauri na unasihi, na viongozi wa shule kuwa sehemu ya mikakati ya kulinda wanafunzi.



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii