Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dkt. Caroline Damian amezindua Kamati ya Ushauri ya Usajili wa Saratani (ACCR) yenye lengo la kuimarisha Usajili wa Saratani nchini kupitia usajili unaozingatia idadi ya watu kwa kuwa na takwimu sahihi.
Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Usajili wa Saratani umefanyika Jijini Dodoma ambapo kamati hii inajumuisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, washirika wa kimataifa kama Vital Strategies, Mtandao wa Usajili wa Saratani Afrika (AFCRN), Shirika la Afya Duniani (WHO) na wawakilishi kutoka katika jamii, akiwemo manusura wa saratani.
Dkt. Caroline amesema kuwa Kamati Kuu itakutana mara mbili kwa mwaka, huku kamati ndogo tano zilizoko Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Kituo cha Tiba Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Kituo cha Tiba cha Kilimanjaro Christian Medical (KCMC), na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, zitakutana kila baada ya miezi mitatu.
“Takwimu sahihi ndiyo msingi wa mipango madhubuti ya sera, programu za kuzuia utambuzi wa mapema, matibabu bora na utunzaji kwa wagonjwa wa saratani,” amesema Dkt. Caroline.