Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche, anatarajia kuongoza Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kesho Mei 23 na 24.
Taarifa iliyotolewa na Chama hicho leo Mei 22 imeeleza kuwa, mara baada ya kufungua kikao, Heche atazungumza na Watanzania.
“Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kuwataarifu viongozi wake, wanachama, na umma wa Watanzania kuwa, tarehe 23 na 24 Mei 2025, kitafanya kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya Chama jijini Dar es Salaam. Kikao hiki kinafanyika kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.15 ya Katiba ya Chama.
Pamoja na ajenda zingine kikao hicho kitajadili ajenda zifuatazo;
1. Hali ya kisiasa nchini
2. Operesheni No Reforms, No Election
3. Uvunjaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa demokrasia nchini
Aidha, mara baada ya ufunguzi wa kikao hicho, Saa 04:00 kamili asubuhi Makamu Mwenyekiti wa Chama - Taifa, Mheshimiwa John Heche, atalihutubia Taifa.”