SERIKALI KUTHIBITI UVUVI HARAMU BAHARI YA HINDI

Serikali imesema imefanikiwa kudhibiti uvuvi haramu kwa kutumia vilipuzi (blast fishing) katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ambapo kwa sasa hali hiyo imedhibitiwa kuanzia vyanzo, wasambazaji na watumiaji wa vilipuzi.

Imesema kwa zaidi ya mwaka sasa hakuna matukio ya uvuvi huo haramu yaliyoripotiwa wala kubainika kwenye ukanda wote wa Bahari ya Hindi.
Hayo yameelezwa bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Mei 23, 2025 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk Ashatu Kijaji wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema wizara imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji ili uhalifu huo usiendelee siku zijazo na kuhakikisha uharamia huo unadhibitiwa kwa kulinda rasilimali za Taifa Vilevile kwa upande wa Maziwa Makuu, Dk Kijaji amesema Serikali imeendelea kusafisha na kuondoa zana haramu za uvuvi.

Amefafanua kuwa kazi hiyo imefanikisha kugundua na kunasa mtandao mpana wa uingizaji wa nyavu haramu. Mafanikio yote yanayopatikana yanatokana na ushirikishwaji thabiti wa wadau mbalimbali wa Sekta ya Uvuvi wakiwemo Viongozi wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (Beach Management Units - BMUs) na Asasi Zisizo za Kiserikali (NGOs).

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii