Bodi ya Utendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kamati ya Kanda ya Afrika, imemkumbuka Dk Faustine Ndugulile na kutuma salamu za rambirambi kwa familia na nchi ya Tanzania kwa kumpoteza kiongozi huyo.
Hayo yamesemwa leo Jumapili, Mei 18, 2025 wakati wa kikao maalumu cha ana kwa ana cha kamati na bodi hiyo ya utendaji kinachofanyika huko Geneva kwa ajili ya kuteua Mkurugenzi wa Kanda ajaye.
Dk Ndugulile alifariki dunia Novemba 27, 2024 wakati akipatiwa matibabu nchini India, alishinda nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Agosti 27, 2024 katika kikao maalumu cha Kamati ya Kanda ya Afrika kilichofanyika Brazzavile nchini Congo.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho leo Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, Chikwe Ihekweazu ameanza kwa kumwelezea Dk Ndugulile kabla ya kuzungumza masuala mengine muhimu.