Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden (82) amegundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya tezi dume ambayo imesambaa hadi kwenye mifupa yake.
Saratani ni ugonjwa ambao hutokea pindi ambapo ukuaji wa seli mwilini unapotokea katika namna isiyoweza kudhibitiwa na kuenea kwa kasi kwa mujibu wa Shirika la Utafiti wa ugonjwa huo (Cancer Research UK).
Taarifa iliyotolewa jana Jumapili kutoka ofisi ya Biden, ilisema kiongozi huyo aliyeondoka madarakani Januari mwaka huu alibaini kuwa siku ya Ijumaa baada ya kuonana na daktari wiki iliyopita kutokana na dalili zilizojionesha katika njia ya mkojo.
Taarifa kutoka kwenye Ofisi yake imeongeza kuwa saratani aliyokuwa nayo Biden haiathiriwi na homoni, hivyo inaweza kudhibitiwa.
Aidha siku ya Jumapili, ofisi ya Biden ilisema aligunduliwa na saratani ya kibofu, yenye alama ya Gleason ya 9 (Daraja la 5) na metastasis kwenye mfupa.
Kutokana na taarifa hiyo, Rais Donald Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa ‘Truth Social’ kuwa yeye na mke wake Melania Trump, "Tunasikitika kusikia kuhusu kilichobainika hivi karibuni wakati wa uchunguzi wa Joe Biden."