LISSU KUACHWA HURU KIZIMBANI

 Mahakama ya Hakimu Kisutu imetoa maelekezo kwa askari wa Jeshi la Magereza kumuacha huru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu akiwa  kizimbani badala ya kumlinda kwa kumzingira ili apate nafasi ya kufuatilia kesi yake kwa uhuru.

Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo Franco Kiswaga ambaye anajukumu la kusikiliza kesi ya uhaini katika hatua ya awali kutokana na hoja zilizotolewa na jopo la mawakili watetezi kutokana upande wa Lissu.
Mawakili hao zaidi ya 20 wakiongozwa na Mpale Mpoki (kiongozi wa jopo), Dk Rugemeleza Nshala, Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya na wengine, wameibua hoja hizo jana Jumatatu, Mei 19, 2025, wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kufahamu kama upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine itakapotajwa tena .
Ambapo baada ya maelezo hayo, ndipo jopo la mawakili hao likaibua hoja kuhusu askari kumlinda Lissu hadi kizimbani ikiwa
Hoja ya ulinzi wa Lissu iliibuliwa na Wakili Nshala kutokana na utaratibu uliotumika kumlinda.

Na kueleza kuwa kawaida mshtakiwa aliye mahabusu akishafikishwa mahakamani hufunguliwa pingu na kuachwa huru kisha hupanda kizimbani peke yake huku Askari wa Magereza wakibaki nje ya kizimba na baada ya kesi kumalizika humfuata mshtakiwa kwa ajili ya kumrudisha mahabusu.

Hata hivyo kwa Lissu leo imekuwa ni tofauti licha ya askari Magereza ,Polisi waliovaa sare na wasio na sare waliokuwepo ndani na nje ya Mahakama askari wengine sita walipanda kizimbani na kumzingira mshtakiwa wakati wote wa kesi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Nshala ameiomba mahakama iamuru askari hao waondoke kizimbani na wasubiri hadi kesi itakapomalizika na kusema kwa mujibu wa Katiba na sheria kila mtu anahesabika kuwa hana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo na mahakama.

Ili kupata taarifa zaidi endelea kutufuatilia kupitia website yetu ya www.jembenijembe.com kupitia Instagram ,Facebook, tikok,x zamani twitter pamoja na YouTube

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii