Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, CPA Amos Makalla amesema kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa awamu ya pili ni fursa nzuri kwa vijana na wananchi kutimiza na kupata haki yao ya kikatiba kwa kushiriki uchaguzi.
Makalla amesisitiza na kusema kuwa awamu hii ni fursa kubwa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 18 na wanatarajia kutimiza umri huo ifikapo Oktoba mwaka huu kwani watapata nafasi ya kutimiza haki kikatiba ya kushiriki uchaguzi kwa kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ili kukidhi vigezo.
Makalla alizungumza hayo Mei 19,2025 wakati akizungumza na wananchi katika Halmashauri ya Wilaya Muleba inayojuisha majimbo mawili ya Muleba Kaskazini na Kusini wakati akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake ya siku saba katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Akiwasalimu wananchi hao Makalla amesema serikali kwa kushirikiana na CCM wapo katika maandalizi ya kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kutimiza takwa la kikatiba na lengo la chama hicho ni kushika dola.
Makalla alisema kuwa ili chama kiweze kushinda kwa kishindo kinahitaji kupigiwa kura na wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakiweka madarakani kwa nguvu ya sanduku la kura ambazo zinapigwa na wananchi.
Akisisitiza hilo kwa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao katika daftari la wapiga kura ambalo utekelezaji wake umeanza Mei 16, mwaka huu na kudumu hadi Mei 22, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi huo.
Makalla ameeleza kuwa kwa upande wa Tanzania bara mchakato huo unafanyika katika mikoa 11 na mikoa mitano kwa upande wa Zanzibar lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanajiandikisha na kuhakiki taarifa zao kwa wale ambao hawakufanikiwa kufanya hivyo hapo awali.
Mikoa hiyo inayopita daftari hilo kwa awamu ya pili ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.