Ugonjwa wa kipindupindu umeua watu 70 ndani ya siku mbili katika mji mkuu wa Sudani, Wizara ya Afya meitangaza leo Alhamisi, Mei 29. Haya yanajiri wakati Khartoum ikikumbwa na kuzorota kwa huduma zake za matibabu. Katika taarifa, wizara imerekodi maambukizo mapya 942 na vifo 25 kwa siu pekee ya Jumatano, kufuatia kesi mpya 1,177 na vifo 45 mnamo siku ya Jumanne.
Mlipuko huo unakuja baada ya wiki kadhaa za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani----zinazohusishwa na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), ambao wamekuwa kwenye vita na jeshi la Sudani kwa zaidi ya miaka miwili- mapigano ambayo yamesababisha kusiishwa kwa usambazaji wa maji na kukatika kwa umeme katika mji mkuu.
Siku ya Jumanne, Wizara ya Afya iliripoti kuongezeka kwa kasi kwa ugonjwa wa kipindupindu, kwa wagonjwa 2,729 na vifo 172 vilirekodiwa katika muda wa wiki moja, huku Jimbo la Khartoum likiwa na asilimia 90 ya maambukizo mapya.
Hata hivyo mamlaka za Sudani zinakadiria kuwa 89% ya wagonjwa, ambao wametengwa, wanapata nafuu, huku wakielezea wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa maji safi, hali ambayo inachochea janga hilo.
Sasa katika mwaka wake wa tatu, vita hivyo vimeua makumi ya maelfu, vimewafanya watu milioni 13 kuyahama makazi yao, na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa "mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu unaoendelea" duniani.