BENKI ya NMB imeikabidhi Wizara ya Kilimo Sh milioni 100 kusaidia maandalizi ya Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kwa jina la Nanenane.
Kiasi hicho ni sehemu ya jumla ya Sh milioni 470 ambazo NMB imefadhili maonesho hayo katika kipindi cha miaka saba. Watakiwa kuchangamkia fursa Nanenane Dodoma
Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango amesema wataendelea kufadhili shughuli za kuimarisha kilimo na ufugaji ili kiwe cha tija zaidi kwa wakulima, wafugaji ili kuimarisha uchumi wa kitaifa.
“Siyo mara ya kwanza kuungana na wakulima, wafugaji na wavuvi, benki hii kupitia NMB Foundation hadi sasa tumeshawafikia vyama vya Ushirika na Amcos zaidi ya 1,500 kwa wakulima wa kahawa, ufuta, tumbaku na korosho,” alisema.
Shango amesema ili Taifa liweze kuimarika lazima watu wake waimarike kifedha na ndiyo maana wanapeleka uwezeshaji kwa walengwa wenyewe. Alisema NMB inalenga kuwatoa wakulima katika kilimo cha mazoea kwenda katika kilimo cha kisasa kitakachowakomboa.
Kwa upande wake, Mkuu wa idara ya Kilimo Biashara Benki ya NMB, Nsolo Mlozi amesema ndani ya benki hiyo wamekuwa na utamaduni wa kutengeneza kalenda kulingana na misimu ya kilimo ikiwemo mkakati wa kuwatoa wakulima katika kilimo cha kutegemea mvua ili wahamie kwenye umwagiliaji.