MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesema mchakato wa Uchaguzi Mkuu haujaathiri kasi ya uwekezaji nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Gilead Teri amesema hali hiyo inaashiria imani ya wawekezaji na Watanzania kwa serikali kwamba, Tanzania ni sehemu salama kuwekeza.
Teri amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uwekezaji nchini katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 Dar es Salaam.
“Hakujakuwa na punguzo la kasi ya uwekezaji na kwenye uchumi tunaitafsiri kama imani ambayo afanyabiashara na wawekezaji kote duniani wanayo juu ya Serikali ya Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba hakutakuwa na changamoto zozote kabla, wakati na baada ya uchaguzi,” amesema.
Teri ametoa wito kwa Watanzania waendelee kuwekeza kwa kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini na
kushirikiana na raia wa kigeni kuwekeza ili kukuza uchumi wa taifa.
Amesema katika kuboresha na kuvutia uwekezaji katika Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZs) imetenga maeneo maalumu ya uwekezaji ambayo ni Bagamoyo, Kwala, Benjamini Mkapa-Mabibo, Nala na Buzwagi na maeneo mengine yaliyotengwa katika mikoa mbalimbali.
“Kampeni hii inalenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta za uzalishaji, huku Watanzania wakipewa fursa ya umiliki wa asilimia 100 au ubia wenye umiliki wa angalau asilimia 30,” amesema Teri.
Amesema wameweka kipaumbele katika sekta 10 zinazozalisha bidhaa za matumizi ya haraka au zinazouzika, kwa uzalishaji wa bidhaa za nguo, uzalishaji wa dawa, utengenezaji na uunganishaji wa magari na vipuri vyake,bidhaa za karatasi na vifaa vya ufungaji na uzalishaji wa mpira na bidhaa zake.
Ametaja sekta nyingine kuwa ni sekta za uzalishaji wa bidhaa za uundaji wa injini za magari, boti, matrekta na pikipiki, kutengeneza mashine rahisi, paneli za nishati ya jua, betri na teknolojia zingine za nishati jadidifu, vifaa vya majumbani na umeme pamoja na samani bidhaa za mbao na vifaa vya ujenzi.
Pia, Teri alisema Tiseza inatekeleza mikakati yake iliyojiwekea, ili kuongeza thamani ya sekta hiyo ambayo ni kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kufuatilia na kufanya tathmini ya miradi ya uwekezaji, kutoa huduma saidizi kwa wawekezaji, kuendeleza maeneo maalumu ya kiuchumi katika mikoa yote na kufanya tafiti za kiuwekezaji na ukusanyaji wa takwimu za mitaji binafsi kutoka nje ya nchi.