JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imefanikiwa kusimamia vyema Itifaki ya Soko la Pamoja katika miaka 25 baada ya kuanzishwa tena mwaka 1999.
Kazi kubwa iliyopo mbele yake kuanzia 2025 ni kusimamia na kutekeleza sarafu ya pamoja, ikiwa ndiyo itifaki inayofuata kabla ya kuhitimisha na shirikisho la kisiasa.
Endapo itifaki ya sarafu ya pamoja itaridhiwa na nchi zote wanachama, kuna manufaa mengi yatakayopatikana ikiwa ni pamoja na biashara kufanyika bila kubadili sarafu mipakani.
Kwa mujibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, itifaki ya sarafu ya pamoja inatarajiwa kukamilika mwaka 2031, ikiwa nchi zote zitapitisha maazimio ya uundwaji wa sarafu hiyo.
Tunaamini kuwa kutokana na mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa itifaki ya soko la pamoja, vivyo hivyo utekelezaji wa itifaki ya sarafu ya pamoja utatimia, ikiwa kutakuwa na ushirikiano wa kutosha.
Hata hivyo, changamoto za mipakani kuhusiana na mazao na bidhaa zimepungua baada ya kuanza kutekelezwa na kusimamiwa vyema kwa itifaki hiyo, ambapo awali ilikuwa changamoto kubwa.
Kutokana na ushirikiano wa kiuchumi kuimarika zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ndio jumuiya kongwe zaidi barani Afrika, inaelezwa kuwa hali hiyo inashajihishwa na usimamizi na utekelezaji mzuri wa Itifaki ya Soko la Pamoja miongoni mwa nchi wanachama.
Moja ya mafanikio makubwa ambayo kila mwananchi wa ndani ya jumuiya anaweza kujivunia waziwazi ni kupanuka kwa jumuiya kutoka nchi tatu za mwaka 1999 hadi kuwa nchi nane mwaka mwaka huu.
Hayo ni mafanikio makubwa, kwa sababu yanaendelea kutafsiri maono ya waasisi wa jumuiya hiyo ambao ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya na Dk Milton Obote wa Uganda, ambao walilenga kuunganisha Bara la Afrika kupitia jumuiya zake.
Pamoja na mafanikio hayo, viongozi wa nchi za EAC wamefanikiwa kutekeleza itifaki mbili kati ya nne ambazo ni Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja, ikiwa bado itifaki ya sarafu moja na Shirikisho la Kisiasa.
Mafanikio hayo yote ni katika kipindi hicho cha miaka 25 na maendeleo ya Sarafu ya Pamoja yanaenda vizuri, kwa sababu taarifa ya Sekretarieti ya EAC chini ya Katibu Mkuu, Veronica Nduva ilisema hadi kufika 2031 itakuwa imekamilika.
Kutekelezwa kwa itifaki ya soko la pamoja na Umoja wa Forodha kumesaidia kuanzishwa miradi mikubwa ya kimkakati ndani ya EAC kama Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, mkoani Tanga na mradi wa barabara za EAC.
Tunaamini kama viongozi wa nchi wanachama wa EAC wataendelea kujituma na kujitolea kuhakikisha itifaki zilizobaki zinatekelezwa, EAC inakuwa ya kwanza duniani kwa kuwa na nguvu na inayoamua mambo yake yenyewe.
Kuna kazi kubwa imefanyika kusaidia nchi zenye changamoto ya machafuko kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini na Somalia, ili kuleta amani ya kudumu kwa njia ya mazungumzo na kwa njia ya kijeshi.
Tunaisihi Sekretarieti ya EAC pamoja na wakuu wa nchi kupitisha mapendekezo ya uundwaji wa sarafu ya pamoja kuwezesha wananchi kufanya biashara bila kulazimika kubadili fedha.