Burkina Faso, Mali na Niger zajiondoa kwenye mahakama ya ICC

Nchi za Mali, Burkina Faso na Niger zinazoongozwa na jeshi, kwa pamoja, zimetangaza kujiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC, kwa kile inachosema Mahakama hiyo yenye makao yake jijini Hague, imekuwa chombo cha ukoloni na inafanya kazi zake kwa upendeleo.

Tamko hilo la pamoja, limetolewa na nchi hizo, ambazo zimeunda umoja wao wa mataifa ya Sahel, na kuishtumu Mahakama ya ICC kwa kushindwa kushughulikia kesi za uhalifu wa kivita na mauaji makubwa na badala yake kutumiwa kuwalenga watu binafsi.

Aidha, nchi hizo zimesema  kuwa uamuzi wa kujiondoa ni njia ya kulinda uhuru wao wa kitaifa, na badala yake yataimarisha mifumo ya ndani ya haki na amani inayozingatia maadili ya kijamii.

Katika hatua nyingine, mataifa hayo, yameahidi kuendeleza kushirikiana na Umoja wa Mataifa na mataifa mengine katika nyanja zinazofaa za haki za binadamu na kuheshimu mamlaka ya kitaifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii