Iran na E3 kukutana kwa mazungumzo muhimu ili kuepusha vikwazo

Iran na mataifa yenye nguvu ya Ulaya yanatayaria kufanya mazungumzo ya dakika za mwisho ili kuzuia kutekelezwa tena kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Tehran, maafisa wawili wakuu wa Iran na wanadiplomasia wawili wa nchi za Magharibi wameliambia shirika la habari la Reuters, ingawa wote wanaonya kuwa uwezekano wa kufaulu bado ni mdogo.

Kwa mujibu wa duru hizo, mawaziri wa mambo ya nje wa IranUingerezaUfaransa na Ujerumani watakutana leo Jumanne pembezoni mwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujadili azma tata ya nyuklia ya Iran, huku kukiwa na vitisho vya kuwekewa vikwazo.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, zinazojulikana kama E3, zilianzisha mchakato wa siku 30 mnamo tarehe 28 Agosti unaolenga kurudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa, wakiishutumu Tehran kwa kukiuka makubaliano ya mwaka 2015 na mataifa yenye nguvu duniani yaliyolenga kuizuia kutengeneza silaha za nyuklia.

Tehran kwa muda mrefu imekuwa ikishikilia kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya amani.

"Iran imekuwa ikiwasiliana na maafisa kutoka kundi la E3/EU na Rafael Mariano Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA tangu asubuhi hii kwenye Umoja wa Mataifa. Mawazo tofauti yamejadiliwa," afisa mkuu wa Iran amesema.

"Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran atakutana kesho na mawaziri wa mambo ya nje wa E3 na Mwakilishi Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU, Kaja Kallas, na ataendelea na majadiliano."

Afisa mwingine mkuu wa Iran amesema: "Kila mtu anaonekana kufanya kazi" kutatua mzozo wa nyuklia. Wanadiplomasia wawili wa Ulaya wamethibitisha mkutano huo wa Jumanne.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii