Ufaransa kuandaa mkutano wa dharura wa DR Congo, Kinshasa yaomba msaada

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne kutambua "mauaji ya halaiki yanayotekelezwa kimya kimya" katika nchi yake, wakati Ufaransa ikitangaza kuwa itakuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura kuhusu mzozo huo mwezi ujao. 

"Dalili zote za maangamizi yaliyopangwa zipo... Huu sio tu mzozo, lakini mauaji ya halaki yanayotekelezwa kimya kimya ambayo yameathiri watu wa Kongo kwa zaidi ya miaka 30," Rais wa DRC FĂ©lix Tshisekedi amesema wakati wa hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ametoa wito wa kuundwa kwa tume huru ya kimataifa ya uchunguzi ili kusaidia "kuvunja mzunguko wa kutokujali ambao umechochea janga hili kwa miongo kadhaa," pamoja na vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya wale waliohusika na "uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na mauaji ya kimbari" yanayofanywa mashariki mwa nchi.

Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa hivi majuzi uligundua uwezekano wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu "unaofanywa na pande zote" kwenye mzozo huo.

Tajiri wa rasilimali za madini, mashariki mwa DRC imekumbwa na migogoro kwa miongo mitatu.

Ghasia zimeongezeka tangu mwaka 2021 na kuibuka tena kwa kundi linaloipinga serikali la M23, linaloungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda na jeshi lake, kulingana na Umoja wa Mataifa.

M23 walichukua udhibiti wa miji mikubwa ya Goma mnamo mwezi Januari na Bukavu mnamo mwezi Februari. Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano tangu mwezi Januari yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na mamia kwa maelfu kuyahama makazi yao.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza Jumanne kwamba Ufaransa itaandaa mkutano wa dharura mwezi Oktoba kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini DRC.

"Katika eneo la Maziwa Makuu, mamlaka na uadilifu wa eneo la DRC lazima uheshimiwe," ametangaza.

"Lazima turudishe matumaini kwa watu wa Kivu na mamia ya maelfu ya watu ambao wamehamishwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo."

Waangalizi wanahofia mashambulizi ya M23 dhidi ya Uvira, mji wa watu 500,000 katika mkoa w Kivu Kusini, ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi la Kongo na wanamgambo wanaounga mkono Kinshasa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii