RC Chalamila apiga marufuku mabaunsa kutumika kwenye migogoro ya nyumba

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemtembelea mama mjane Alice Haule, ambaye anadaiwa kufukuzwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi maeneo ya Mikocheni, nyumba inayodaiwa kuwa sehemu ya urithi kutoka kwa marehemu mumewe, Justice Rugaibula.

Katika ziara hiyo, RC Chalamila ameambatana na viongozi wa serikali, maafisa wa ardhi na Jeshi la Polisi kwa lengo la kusikiliza malalamiko ya mama huyo, ambaye amekuwa akipitia changamoto za kifamilia na kisheria tangu kufariki kwa mumewe mwaka 2022.

Akizungumza baada ya kupata maelezo ya pande zote, Chalamila amesema kitendo cha kumvunjia mtu nyumba na kumtoa kwa nguvu ni udhalilishaji mkubwa na hakiwezi kuvumiliwa. Aliweka wazi kuwa kuanzia sasa matumizi ya mabaunsa katika kushughulikia migogoro ya ardhi na nyumba ni marufuku, akisisitiza kuwa jukumu hilo ni la polisi pekee.

“Kuanzia sasa ni marufuku kutumia mabaunsa kufukuza watu kwenye nyumba. Watakaoendelea na vitendo hivyo watakamatwa mara moja. Polisi wapo kwa kazi hiyo na si watu binafsi,” amesema Chalamila.

Ameongeza kuwa hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa hadi ukweli wa suala hilo ubainike, kwani upande wa mjane Alice Haule na mfanyabiashara Mohamed Yusuph Ali wote wanadai umiliki wa nyumba hiyo.

Kwa upande wake, Alice Haule amesema alinunua nyumba hiyo mwaka 2007 akiwa na mumewe, lakini baada ya kifo cha mumewe alianza kukumbwa na vitisho na mashinikizo kutoka kwa Mohamed Yusuph, ambaye anadai alinunua nyumba hiyo kwa zaidi ya Sh milioni 160. Alice anadai hakuwa sehemu ya mauziano hayo na tangu wakati huo amekuwa akipitia mateso, yakiwemo vitisho, kuvamiwa, kukatiwa umeme na kufukuzwa bila taarifa rasmi.

“Licha ya kufungua kesi mahakamani, sijawahi kupata haki. Sasa ninaishi kwa wasiwasi mkubwa,” amesema Alice kwa uchungu.

Kwa upande wake, Wakili wa Mohamed Yusuph, Hajira Mngura, amesema mteja wake alinunua nyumba hiyo kihalali mwaka 2011 kutoka kwa marehemu, na kwamba nyaraka zote za kisheria zipo. Aidha, alidai kuwa ili mgogoro huo umalizike, Alice alitakiwa kumlipa Sh milioni 500 kama fidia lakini hakufanya hivyo.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukrani Kyando, amebainisha kuwa rekodi za ardhi zinaonyesha nyumba hiyo ilimilikishwa kwa marehemu na baadaye kuuzwa kwa Mohamed Yusuph kwa kufuata taratibu za kisheria, ingawa mke wa marehemu aliwahi kupinga mauzo hayo akiwa hai.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni amesema alipokea taarifa za mgogoro huo kwa simu kutoka kwa mlalamikaji na aliagiza kusitishwa hatua zote hadi uchunguzi ukamilike.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mtatiro Kitilo, amesema baada ya malalamiko ya mama huyo walitoa agizo la kukamatwa kwa wote waliohusika katika uvamizi huo, huku uchunguzi wa nyaraka ukiendelea.

“Vitendo vya kutumia mabavu, mabaunsa na ukiukwaji wa haki haviwezi kuvumiliwa. Polisi tumeanza uchunguzi na hatua zitachukuliwa kwa wote waliohusika,” amesema Kamanda Mtatiro.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii