Mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 24, 2025 ameshiriki sala fupi na kuweka shada la maua katika kaburi la Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, kijijini Lupaso, Masasi mkoani Mtwara.
Kabla ya sala hiyo iliyoongozwa na Padri Cyril Massawe, Dk. Samia aliwasha mshumaa na kisha kumwombea hayati Mkapa pamoja na familia yake. Padri Massawe pia alimwombea Dk. Samia ili Mungu amjalie nguvu na ulinzi katika kuendelea kuongoza taifa na katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi.
Dk. Samia alipokelewa na wanafamilia wa hayati Mkapa akiwamo Nicholas Mkapa, William Erio na Chifu Nkonona Mkapa V. Ziara hiyo ni sehemu ya kampeni zake katika Mkoa wa Mtwara.