Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda zimekubali kuanza kutekeleza hatua za kiusalama chini ya makubaliano yaliyoidhinishwa na Marekani mwezi ujao, vyanzo vitatu vinavyofahamu suala hilo vimeliambia shirika la habari la Reuters. Hii ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa makubaliano ya amani, licha ya wasiwasi kuhusu ukosefu wa maendeleo.
Nchi hizo zimekubali kukamilisha hatua hizo ifikapo mwisho wa mwaka, vyanzo hivyo vimesema. Utekelezaji utaanza Oktoba 1, na operesheni za kuondoa tishio lililoletwa na kundi la wapiganaji la Kongo, Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), na kuwezesha kuondoka kwa wanajeshi wa Rwanda zitaanza kati ya Oktoba 21 na 31, duru hizo zimesema.
Muda huo, uliochapishwa awali na Reuters, unatoa tarehe maalum kwa Rwanda na Kongo kutekeleza mpango wa amani, licha ya wasiwasi kuhusu matatizo yaliyojitokeza.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Kongo na Rwanda walitia saini makubaliano ya amani mjini Washington Juni 27 na kukutana siku hiyo hiyo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye ana nia ya kuvutia mabilioni ya dola katika uwekezaji wa nchi za Magharibi katika eneo lenye utajiri wa tantalum, dhahabu, kobalti, shaba, lithiamu na madini mengine.
Makubaliano hayo yalijumuisha dhamira ya kutekeleza makubaliano ya mwaka 2024 yanayoeleza kuwa Rwanda itaondoa hatua za kujihami ndani ya siku 90.
Operesheni za kijeshi za Kongo zinazolenga kundi la FDLR, kikundi chenye silaha chenye makao yake makuu Kongo ambacho kinajumuisha mabaki ya jeshi la zamani la Rwanda na wanamgambo waliohusika na mauaji ya halaiki ya 1994, zimepangwa kumalizika wakati huo huo.
Vyanzo hivyo vimesema wahusika wataanza kutekeleza hatua hizo mnamo Oktoba 1, ingawa tarehe ya mwisho ya siku 90 iliyowekwa katika makubaliano ya 2024 inaangukia siku ya Alhamisi.
Chanzo kimojawapo kimesema muda haukuanza na kutiwa saini kwa mkataba huo, lakini ulipangwa kuanza na mkutano wa kwanza wa utaratibu mpya wa uratibu wa usalama wa pamoja mnamo Agosti 7-8.
Msemaji wa serikali ya Rwanda, msemaji wa serikali ya Kongo, na Wizara ya Mambo ya Nje hawakutoaa maoni yoyote ya mara moja.