Ufaransa iko tayari kuunda ndege ya kivita ya siku za usoni ikiwa peke yake ikiwa mazungumzo na Berlin na Madrid yatashindwa kuhusu mradi wa baadaye wa ndege ulioandaliwa kwa pamoja, afisa wa Ufaransa amesema siku ya Jumatano, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina. Mfumo wa vita vya anga wa baadaye, mradi wa SCAF, uliozinduliwa mnamo mwaka 2017 na Ufaransa na Ujerumani, kisha ukaunganishwa na Uhispania, sasa unaonekana kuwa katika hali mbaya.
Kwa utaalam wake unaotambulika, jampuni ya kutengeneza ndege ya Ufaransa Dassault hapo awali iliteuliwa kuongoza muundo wa ndege. Kampuni tanzu ya Ujerumani ya Airbus inaongoza kwenye mfumo huu na ndege zisizo na rubani ambazo zitaandamana na ndege hii ya kivita ya siku zijazo. Usawa huu kati ya Ujerumani na Ufaransa umedhoofishwa na kuwasili kwa kampuni tanzu ya Uhispania ya Airbus katika mradi huo. Katika nafasi ya nguvu, Airbus, ambayo kwa hiyo inawakilisha maslahi ya Berlin na Madrid, haina nia ya kutoa makubaliano mengi sana kwa kampuni ya Kifaransa.
Berlin na Madrid zimekasirishwa sana na msimamo wa Dassault, zikidai uhuru zaidi katika jukumu lake kama mkandarasi mkuu wa viwanda, ambalo liliteuliwa na mataifa hayo matatu. Kampuni hiiya Ufaransa inadai haki ya kuchagua wakandarasi wake wadogo, hata ikiwa inamaanisha kubadilisha mzigo wa kazi kwa theluthi moja iliyopangwa kwa kampuni za kutengeneza ndege kutoka kila nchi.
Lakini wakati unaenda. Hatua muhimu ya kuunda ndege hiyo itaanza mnamo mwaka 2026. Mivutano inaongezeka kati ya kampuni hizo na nchi hizi tatu. Bloomberg ilifichua siku chache zilizopita kwamba Berlin inafikiria kuiondoa Ufaransa katika mradi wa SCAF ili kuunga mkono makubaliano ya ushirikiano na Sweden au Uingereza, au hata kwenda peke yake na Uhispania.
Jibu kutoka kwa Eric Trappier, Mkurugenzi Mtendaji wa Dassault, lilikuwa la haraka. "Sekta ya Ufaransa," alibainisha siku ya Jumatatu, Septemba 22, "ina ujuzi na utaalamu wote wa kutengeneza ndege ya kizazi kipya peke yake." Mgogoro huo ni wa kweli, na mipango mikuu ya kimuundo ya Ufaransa na Ujerumani, kama vile SCAF, sasa iko kwenye hatihati ya kuporomoka.
Wakati wa ziara yake mjini Madrid wiki iliyopita, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisema kuwa Ujerumani na Uhispania zilitaka "kujaribu kufikia suluhu ifikapo mwisho wa mwaka wa 2025." Mkutano kati ya mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo tatu umepangwa kufanyika Oktoba ili kuendelea.
"Tuna maoni sawa: hali ya sasa si ya kuridhisha. Hakuna maendeleo yoyote katika mradi huu," Kansela wa Ujerumani alitangaza pamoja na mwenzake wa Uhispania, Pedro Sanchez. Kwa afisa huyo wa Ufaransa, "leo, hakuna aliyefaulu kuonyesha kwamba shirika la sasa la SCAF linaruhusu uundaji wa ndege ambayo inakidhi mahitaji makubwa ya Ufaransa kwa wakati unaofaa."