Donald Trump asema 'hataruhusu Israel kuteka Ukingo wa Magharibi'

Donald Trump amebainisha siku ya Alhamisi, Julai 25, kwamba "hataruhusu Israel kutwaa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu," hatua iliyotakiwa na mawaziri wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Israel kulipiza kisasi kwa kutambuliwa kwa taifa la Palestina na nchi kadhaa.

"Sitairuhusu Israel kunyakua Ukingo wa Magharibi. Hapana, sitairuhusu. Haitatokea," amesema rais wa Marekani, ambaye alikuwa bado hajatangaza hadharani  msimamo wake kuhusu suala hilo, kabla ya kurudia: "Sitairuhusu Israel kutwaa Ukingo wa Magharibi. Hiyo inatosha. Ni wakati wa kusitisha sasa."

Amehakikisha tena kwamba makubaliano kuhusu Gaza yako "karibu kabisa kufikiwa," akisema alizungumza na Benjamin Netanyahu wakati wa mchana. "Tunakaribia kabisa kuwa na makubaliano kuhusu Gaza na pengine hata amani," rais wa Marekani amesema.

Hayo yanajiri wakati Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ameshtumu mauaji yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

"Uhalifu dhidi ya ubinadamu" unaofanywa na Israel huko Gaza ni "moja ya sura za kutisha" za karne ya 20 na 21, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ametangaza katika hotuba ya video kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

"Kinachofanywa na Israel sio uchokozi tu, ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu (...) ambao utarekodiwa katika kurasa za vitabu vya historia na katika dhamiri ya ubinadamu kama moja ya sura za kutisha zaidi za maafa ya kibinadamu ya karne ya 20 na 21," ametangaza kiongozi huyo, ambaye alinyimwa visa na Marekani.

Kwa upande mwingine jeshi la Israel limetangaza siku ya Alhamisi kuwa Wapalestina 700,000 wameukimbia Mji wa Gaza hadi kusini mwa Ukanda wa Gaza tangu mwishoni mwa mwezi wa Agosti, huku kukiwa na mashambulizi ya ardhini ya wanajeshi wa Israel katika mji huo kwa lengo la kuangamiza Hamas.

"Wapalestina laki saba wamehama," jeshi limesema likijibu swali la shirika la habari la AFP kuhusu idadi ya watu waliokimbia mji wa Gaza tangu mwisho wa mwezi wa Agosti, wakati Umoja wa Mataifa ulikadiria idadi ya watu huko kuwa karibu milioni moja.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii