Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Arthur Nanauka, amezitaka Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote nchini kutenga bajeti maalum kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya vijana ili kuimarisha utekelezaji wa majukwaa ya vijana katika ngazi za mikoa na wilaya.
Agizo hilo amelitoa leo mkoani Mwanza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform), akisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, taasisi za umma zinapaswa kutenga asilimia 10 kwa ajili ya vijana, ikiwa ni sehemu ya asilimia 30 inayotengwa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Waziri Nanauka amewahimiza vijana kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika Jiji la Mwanza, ikiwemo sekta ya uvuvi, ili kujiongezea kipato na kujiinua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, amesema kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa mkoani humo, vijana wazawa wamefanikiwa kupata ujuzi kutoka kwa wataalamu wa ndani na nje ya nchi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ilemela, William Kafiti, ameishauri Serikali kuwekeza zaidi katika miundombinu jengefu ili kuwawezesha vijana kujiajiri na kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na zile zilizopo katika jamii zao.
Sasa ili kupata undani wa taarifa hii tafadhali usikose kutufuatilie na Usikilize jembe Habari Kamili hapo saa moja kamili jioni ambapo msomaji wetu wa hii leo ni Benson Mwakakongole tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime