Watu waliokuwa na silaha wamewaua takriban watu 29 katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria, huku mashuhuda wakisema washambuliaji waliwalenga vijana waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa mpira wa miguu.
Shambulio hilo limetokea katika
jimbo la Adamawa, linalopakana na Cameroon, ambalo kwa miaka mingi limekuwa
likikumbwa na machafuko yanayotokana na shughuli za makundi yenye misimamo
mikali ya kidini pamoja na magenge ya uhalifu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya gavana, Ahmadu Umaru
Fintiri alitembelea eneo la tukio na kuthibitisha kuwa si chini ya watu 29
wameuawa katika shambulio hilo dhidi ya jamii ya Guyaku iliyopo
katika eneo la serikali ya mtaa wa Gombi.
Msemaji wa gavana alieleza kupitia mitandao ya kijamii kuwa
serikali ya jimbo inafanya tathmini ya kina kuhusu tukio hilo na imeahidi
kuimarisha ulinzi katika maeneo yaliyo hatarini.
Gavana Fintiri amewatupia lawama wapiganaji wa kundi linalojulikana kwa mashambulizi yake kaskazini-mashariki mwa Nigeria akisema kuwa tukio hilo linaendana na mbinu zao za kushambulia raia katika maeneo ya vijijini.
Ingawa uchunguzi bado unaendelea, wakazi wanasema washambuliaji walifika kwa ghafla na kufyatua risasi kiholela, wakilenga hasa vijana waliokuwa wakicheza au kutazama mpira.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime