Baada ya miaka kadhaa ya mvutano na majirani zake wa kaskazini, Rais mteule wa Benin Romuald Wadagni amefanya ziara nchini Niger na Burkina Faso siku ya Jumanne, Juni 2, ambapo alikutana na Jenerali Abdourahamane Tiani na Kapteni Ibrahim Traoré. Lengo la ziara hizi: "kutoa msukumo mpya kwa uhusiano wa muda mrefu" unaounganisha nchi hizo tatu na kushughulikia masuala wanayoshiriki, hasa katika sekta za kiuchumi na usalama.
Uhusiano kati ya Benin na majirani zake katika Muungano wa mataifa ya Sahel, Alliance of Sahel States (AES), ulipiga hatua mbele siku ya Jumanne, Juni 2. Siku kumi tu baada ya kuapishwa kwake, rais mpya wa Benin aliendelea na ziara yake ya kikanda Afrika Magharibi kwa kuzuru Niger na Burkina Faso. Lengo lake: kuanzisha tena mazungumzo na nchi mbili ambazo Benin ilikuwa imepitia kipindi kirefu cha mvutano nazo hivi karibuni.
Romuald Wadagni alitua kwa mara ya kwanza huko Niamey. Alipokelewa kwenye uwanja wa ndege na Jenerali Abdourahamane Tiani, alipokelewa kwa heshima kubwa, ya kidugu na ya kirafiki, kulingana na taarifa ya mwisho ya pamoja, ambayo pia ilibainisha nia ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano kati ya majirani hao wawili.
Viongozi hao wawili waliahidi "kufanya kazi ya kuondoa vikwazo vyote kwa minajili ya kuimarisha ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kufunguliwa tena kwa mpaka wa Niger-Benin," ambao ulifungwa kufuatia mapinduzi nchini Niger mwaka 2023 na haujafunguliwa tena tangu wakati huo, kulingana na hati hiyo. Kamati ya wataalamu iliyopewa jukumu la kutambua na kushughulikia vikwazo hivi inatarajiwa kuwasilisha ripotiyake ndani ya siku 15.
Mada nyingine muhimu iliyojadiliwa na Romuald Wadagni na Jenerali Tiani ni usalama, wakati Sahel na maeneo ya kaskazini mwa nchi za pwani yanakabiliwa na mashambulizi ya makundi ya kijihadi. Mkuu wa nchi wa Benin aliambatana na mshauri wake maalum kuhusu usalama na ulinzi, mkuu wa idara ya ujasusi, na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje. Viongozi hao wawili waliahidi kuunganisha nguvu ili kupambana na ugaidi na ujambazi.
Mchana, Romuald Wadagni kisha alisafiri hadi Ouagadougou ambapo alishiriki katika kikao cha kazi katika ikulu ya Koulouba na Kapteni Ibrahim Traoré. Kulingana na taarifa ya mwisho ya pamoja, ziara hii ya kirafiki na ya kikazi ililenga "kuimarisha uhusiano wa muda mrefu" kati ya Benin na Burkina Faso na kujenga ushirikiano mpya "unaotegemea uaminifu, heshima ya pande zote, na kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazokabili nchi hizi mbili."
Viongozi wa Niger na Burkina Faso walialikwa Cotonou. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni hali ya usalama. Katika suala hili, Romuald Wadagni na Kapteni Ibrahim Traoré walisisitiza "hitaji muhimu" la kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa jirani katika kukabiliana na ugaidi, uhalifu uliopangwa, na aina zote za itikadi kali za kikatili.
Katika upande wa kiuchumi, umuhimu wa bandari ya Cotonou katika kusambaza bidhaa na huduma kwa Burkina Faso ulisisitizwa, na kuwafanya viongozi hao wawili kujitolea kuimarisha ushirikiano wao katika suala la uchukuzi na usafirishaji, pamoja na kuhimiza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili. Tume ya Ushirikiano wa Pamoja kati ya Burkina Faso na Benin itazinduliwa haraka iwezekanavyo.
Kama mwenzake wa Niger, Kapteni Ibrahim Traoré pia amealikwa Cotonou na amekubali mwaliko huo. Tarehe za ziara za viongozi hao wawili nchini Benin zitatangazwa baadaye kupitia njia za kidiplomasia.