Idadi kubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu wamekusanyika leo katika uwanja wa Arafat, hatua inayotajwa kuwa kilele cha ibada ya Hajj na moja ya siku tukufu zaidi katika kalenda ya Kiislamu.
Kuanzia alfajiri, maelfu ya mahujaji waliovalia mavazi meupe ya "Ihram" walifika katika eneo hilo lililoko karibu na mji wa Makkah.
Katika Mlima Arafat, wenye urefu wa takriban mita 70, mahujaji walitekeleza ibada ya Wuquf Arafah, sehemu muhimu ambayo inaaminika kuwa Mtume Muhammad alitoa hotuba yake ya mwisho.
Mwaka huu, zaidi ya watu milioni 1.5 wanaripotiwa kushiriki ibada ya Hajj licha ya mazingira ya wasiwasi yaliyosababishwa na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Baada ya kusimama Arafat, mahujaji wataelekea Muzdalifah, ambako watakusanya kokoto zitakazotumika katika ibada nyingine ya Jamrat—kitendo cha kurushia mawe nguzo zinazoashiria shetani katika eneo la Minaa. Ibada hiyo inatarajiwa kuanza kesho Jumatano.