Ajali za majini zimeendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazohatarisha maisha ya maelfu ya wananchi wanaotegemea Ziwa Victoria kwa shughuli za kila siku.
Wavuvi, wafanyabiashara, wanafunzi na wasafiri hukatiza mawimbi ya ziwa hilo kila siku, wakiamini watafika salama wanakoelekea. Hata hivyo, pale ajali zinapotokea, mafanikio ya operesheni za uokozi hutegemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa boti maalumu za uokozi na mfumo wa mawasiliano unaofanya kazi kwa haraka.
Ni katika muktadha huo ndipo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ametoa rai kwa wananchi, hususan watumiaji wa Ziwa Victoria, kuhifadhi namba za mawasiliano ya vikosi vya uokozi ili kurahisisha utoaji wa taarifa za dharura na kuongeza nafasi ya kuokoa maisha.
Mhe. Mtanda amesema bado kuna baadhi ya wananchi wanaopuuzia umuhimu wa kuhifadhi namba muhimu za dharura, hali inayosababisha ucheleweshaji wa taarifa pindi ajali zinapotokea.
“Dakika chache zinazopotea kabla taarifa haijafika kwa vikosi vya uokozi zinaweza kuwa tofauti kati ya maisha na kifo,” amesema Mtanda.
Somo la ajali ya MV Kalebezo
Ajali ya boti ya MV Kalebezo imekuwa ushahidi halisi wa umuhimu wa boti za uokozi katika kukabiliana na majanga ya majini.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, mara baada ya taarifa za ajali kupokelewa kupitia kituo cha mawasiliano ya dharura, boti za uokozi za Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) zilielekezwa eneo la tukio ndani ya muda mfupi na kuanza operesheni ya kuwaokoa manusura.
Kwa Mhe. Mtanda, mwitikio huo wa haraka usingewezekana bila uwekezaji uliofanywa na Serikali katika boti za kisasa za uokozi pamoja na mfumo wa kisasa wa kupokea na kuratibu taarifa za dharura.
Anasema tukio hilo limeonesha wazi kuwa boti za uokozi si vifaa vya kusubiri kutumika mara chache, bali ni nyenzo muhimu zinazoweza kuamua hatima ya maisha ya watu wakati wa majanga.
Boti za uokozi zimeongeza kasi ya mwitikio wa kuwafikia wahanga wa ajali za majini tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo waokoaji walitegemea vyombo vya kawaida kufika eneo la ajali, sasa Serikali imeweka boti maalumu zenye uwezo wa kufika haraka kwenye maeneo yenye dharura.
Boti hizo zimeboreshwa kwa vifaa vinavyowezesha kufanya operesheni za utafutaji na uokoaji katika mazingira magumu ya Ziwa Victoria.
Mbali na kuokoa manusura, boti hizo hutoa msaada wa kwanza kwa waathirika na kuwahamisha haraka kutoka eneo la ajali hadi sehemu salama.
Kwa mazingira ya Ziwa Victoria, ambako hali ya hewa inaweza kubadilika ghafla na mawimbi kuwa makubwa, uwepo wa boti maalumu za uokozi umeongeza uwezo wa Serikali kuwafikia wahanga kwa muda mfupi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Boti ya Matibabu ‘Ambulance Boat’ imeleta mapinduzi kwenye huduma za dharura
Mbali na boti za uokozi, Serikali imewekeza pia katika ‘Ambulance Boat’, chombo maalumu kinachotoa huduma za dharura kwa wagonjwa na majeruhi waliopo ndani ya ziwa.
Kwa wakazi wa visiwani, huduma hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwani wagonjwa hawalazimiki tena kusubiri usafiri wa kawaida kabla ya kufikishwa hospitalini.
Katika ajali za majini, dakika za mwanzo baada ya tukio huwa muhimu sana. Ambulance Boat inasaidia kuhakikisha majeruhi wanapata huduma za kitabibu kwa haraka na kuongeza uwezekano wa kuokoa maisha yao.
Mwanza inahitaji uwekezaji mkubwa katika uokozi
Mhe. Mtanda amesema umuhimu wa boti za uokozi unatokana pia na jiografia ya Mkoa wa Mwanza. Ameeleza kuwa takribani asilimia 53 ya eneo la mkoa huo ni maji huku asilimia 47 pekee ikiwa nchi kavu.
Kutokana na hali hiyo, maelfu ya wananchi hutegemea usafiri wa majini kila siku kwa shughuli za kiuchumi, ikiwemo uvuvi, biashara, usafirishaji wa bidhaa na utalii.
Hivyo, usalama wa majini hauwezi kutenganishwa na maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Mwanza.