Takriban watu wanane wauwawa na wengi kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanyika dhidi ya miji mbali mbali ya Ukraine huku Rais Zelensky akiwashinikiza washirika wake kumtumia mifumo ya ulinzi wa anga.
Umoja wa Ulaya umeikosoa Urusi kwa kuishambulia tena Ukraine na kusema kwamba mashambulizi hayo yamekiuka anga ya Poland.
Maafisa wa Ukraine wamefahamisha kwamba Urusi ilianzisha mashambulio makubwa usiku wa kuamkia leo dhidi ya nchi hiyo na kusababisha vifo vya takriban watu wanane na kujeruhi wengine wengi. Miji kadhaa ya Ukraine ikiwemo ya upande wa Magharibi kutoka mpakani mwa Urusi ililengwa kwa makombora na mamia ya droni. Tahadhari za mashambulizi ya anga zilitolewa kote nchini humo.Zelensky aelezea matumaini ya Ukraine kujiunga na EU
Rais Volodymry Zelensky amesema makaazi ya watu,biashara na miundo mbinu imeharibiwa vibaya na Urusi ambayo imefyetuwa zaidi ya makombora 70 ikiwemo ya masafa marefu na droni 280.
Zelensky kwa mara nyingine amewatolea wito washirika wake wa nchi za Magharibi na hasa Marekani kuipatia nchi yake mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot.