DED Kibiti akamata gari linalosafirisha mchanga bila risiti

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ramadhan Kimara, amekamata gari lililokuwa likisafirisha mchanga kutoka kwenye shimo la mchanga bila kuwa na risiti ya malipo ya ushuru, wakati wa ukaguzi wa vyanzo vya mapato katika wilaya hiyo.

Kimara amekamata gari hilo Oktoba 14, 2026, alipofanya ziara ya kukagua vyanzo mbalimbali vya mapato ya halmashauri na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya watendaji wanaohusika na ukusanyaji wa mapato.

Katika ukaguzi huo, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha malipo ya ushuru yanafanyika kwa kufuata taratibu zilizowekwa na kurekodiwa katika mfumo rasmi wa ukusanyaji mapato.

Amesema ukaguzi huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi wa mapato na uwajibikaji wa watendaji, ili fedha zinazokusanywa zitumike katika kuboresha huduma na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Kibiti.

Katika hatua nyingine, mwanzoni mwa wiki hii Kimara alikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkupuka, iliyopo Kijiji cha Mkupuka, unaotarajiwa kugharimu Sh milioni 528.

Akiwa katika eneo la mradi, alizungumza na fundi pamoja na msimamizi wa ghala la vifaa vya ujenzi, akiwataka kuhakikisha vifaa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kazi inakamilika ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba.

Aidha, amemtaka mhandisi wa mradi kutembelea eneo la ujenzi mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya kazi na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza na kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii