Balozi wa Marekani Afunguka Hatma ya Netanyahu Kuunda Serikali

Balozi wa Marekani nchini Israel, Mike Huckabee, amesema matokeo ya uchaguzi nchini Israel yaliyoonesha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kupata uungwaji mkono mkubwa kuliko ilivyotarajiwa yamebadilisha mwelekeo wa siasa za nchi hiyo, huku hatua inayofuata ikiwa ni mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Newsmax, Huckabee amesema kambi ya Netanyahu imepata viti 53, ikilinganishwa na viti 48 vya kambi ya kiongozi wa upinzani Eisenkot, lakini hakuna upande uliofikia viti 61 vinavyohitajika ili kupata wingi wa kuunda serikali katika Bunge la Israel lenye viti 120.

Amesema matokeo hayo yalikuwa tofauti na matarajio ya wengi waliodhani kuwa kambi ya mabadiliko ingeibuka na ushindi katika uchaguzi huo.

Huckabee ameeleza kuwa hatua inayofuata itakuwa ni Rais wa Israel kumpa Netanyahu au Eisenkot nafasi ya kwanza ya kujaribu kuunda serikali, ambapo watakuwa na siku 42 za kutafuta uungwaji mkono wa wabunge wasiopungua 61.

Amesisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi pekee hayaamui nani atakuwa Waziri Mkuu, bali uwezo wa kiongozi kupata washirika wa kutosha kuunda serikali.

Serikali ya umoja na nafasi ya vyama vya Waarabu

Akizungumzia uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kati ya Netanyahu na Eisenkot, Huckabee amesema kauli zinazotolewa na wanasiasa wakati wa kampeni hazipaswi kuchukuliwa kuwa msimamo wa mwisho wakati wa mazungumzo ya kuunda serikali.

Amesema baadhi ya wanasiasa wanaweza kubadili misimamo yao wanapokabiliwa na uwezekano wa kubaki nje ya serikali kwa kipindi cha miaka minne.

Hata hivyo, kuhusu msimamo wa Netanyahu wa kutovitaka vyama vya Waarabu katika serikali yake, Huckabee ameuelezea kuwa ni muhimu, akitoa hoja kuhusu baadhi ya kauli za wanasiasa wa Kiarabu kuhusu Israel na shambulio la Hamas la Oktoba 7.

Kwa mujibu wa Huckabee, vyama vya Waarabu vilipata viti 19 katika uchaguzi huo, lakini amesema baadhi ya wanasiasa waliochaguliwa wamekuwa na misimamo inayozua maswali kuhusu ushiriki wao katika serikali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii