Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Prince Faisal bin Farhan Al Saud, amefanya mazungumzo ya njia ya simu mwenzake wa Iran, Abbas Araghchi, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la serikali ya Saudi Arabia.
Mawaziri hao wawili wamejadili kuhusu kuongezeka kwa mvutano katika eneo la mashariki ya kati hivi karibuni baada ya kundi la Houthi, linaloungwa mkono na Iran, kushambulia viwanja vya ndege vya Saudi Arabia.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa Telegram siku ya Jumapili, Araghchi alisisitiza kuwa matumizi ya nguvu za kijeshi bila kuzingatia suluhu za kisiasa kutazidisha zaidi mzozo na kufanya hali kuwa mbaya.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa Iran, migogoro kwenye ukanda wa mashariki ya kati haina suluhu la kijeshi.
Wiki iliyopita, Araghchi alisema kuwa hakuna suluhu ya kijeshi kwa vita vya Iran na Marekani, akiongeza kuwa mazungumzo pekee yanayozingatia haki na usawa ndiyo yanaweza kumaliza mgogoro huo.
Araghchi alisema Iran iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika ili kuwezesha kufanyika kwa mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Yemen na kusaidia kufikia suluhu ya kisiasa.
Kwa upande mwengine, baada ya shambulio baya kwenye uwanja wa ndege jijini Riyadh nchini Saudi Arabia, Rais wa Marekani Donald Trump alidai kuwa angefikiria upya nafasi ya Marekani nchini Yemen, akiongeza kuwa anatafakari uwezekano wa kuanza tena mashambulizi dhidi ya Iran.
Zaidi ya watu 10 waliripotiwa kuawa kwenye shambulio hilo la waasi wa Houthi katika uwanja wa ndege jijini Riyadh, karibia watu 300 wakijeruhiwa.