Wizara ya Afya ya Kenya yasema hakuna mgonjwa wa Ebola aliyegunduliwa tangu kifo cha mgonjwa aliyeingia kutoka DRC.
Kenya imesema haijabaini kisa kingine chochote kipya cha ugonjwa wa Ebola baada ya kufanya vipimo 293 tangu mgonjwa wa kwanza wa homa hiyo hatari alipoaga dunia mnamo Oktoba 5 wakati akipatiwa matibabu mjini Nairobi.
Hayo yameelezwa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo ambayo pia imearifu kwamba watu 108 kati ya 122 walioorodheshwa kuwa walikutana na mgonjwa aliyepoteza maisha wamewekwa karantini na hadi sasa hakuna mwenye dalili za Ebola.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilithibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola tarehe 06 Oktoba pale raia wake mmoja aliyewasili kutokea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuugua na kufariki kwa ugonjwa huo.
Wizara ya Afya imewahimiza wananchi kuendelea kuwa watulivu na iwapo mtu atahisi kuwa na dalili za Ebola kutafuta msaada wa matibabu haraka iwezekanavyo.
Kenya ni miongoni mwa nchi zilizoripoti visa vinavyohusishwa na mlipuko unaoendelea mashariki mwa DRC, ambao umeelezwa kuwa miongoni mwa milipuko mikubwa zaidi ya Ebola kuwahi kurekodiwa.