Mshukiwa wa mauaji ya kimbari arejeshwa Rwanda kutoka Marekani

Raia wa Rwanda aliyekuwa amefungwa nchini Marekani kwa kosa la kusema taarifa za uongo kuhusu ushiriki wake kwenye mauaji ya kimbari mwaka 1994, amefukuzwa nchini humo na kurejeshwa Kigali.

Jean Leonard Teganya, mwenye umri wa miaka 55, alipatikana na hatia hiyo Aprili mwaka 2019 kwa kuwadanganya maafisa wa uhamiaji nchini Marekani kuhusu ushiriki wake kwenye mauaji ya kimbari ili aruhusiwe kuwa mkimbizi.

Alifungwa jela miezi 97 na baada ya adhabu hiyo alitakiwa kufukuzwa nchini Marekani, kitendo ambacho kimefanyika na kuthibitishwa na ofisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma nchini Rwanda.

Imebainika kuwa, wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Teganya alikuwa mwanafunzi wa Udaktari katika chuo cha taifa cha Rwanda na mwanchama wa chama cha siasa cha MRND kinachohusishwa na Wahutu wanaotuhimiwa kuhusika pakubwa kwenye mauaji hayo.

Nchini Rwanda, Teganya, anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika na mauaji ya Watustsi saba na kuwabaka wanawake wawili, kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama zinazoonesha kuwa aliwapeleka wauaji hospitalini kuwasaka wagonjwa wa Kitutsi na wakimbizi waliouawa kipindi hicho cha mauaji ya kimbari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii