Joto la dunia laendelea kupanda

Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaendelea mjini Antalya, huku viongozi, wataalamu wa mazingira na wadau mbalimbali wakijadiliana hatua za kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

Mkutano huo uliofunguliwa Jumatatu (Novemba 9) umejikita katika maeneo matatu makuu ambayo ni utekelezaji wa malengo ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi, upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea, pamoja na kuimarisha mikakati ya uhimilivu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mikutano ya COP, mkutano huo unaendeshwa chini ya mfumo wa uongozi wa pamoja, ambapo Uturuki ni mwenyeji wa mkutano huku Australia ikiongoza mazungumzo rasmi ya nchi wanachama.

Katika siku za mwanzo za mkutano huo, viongozi wamezitaka takribani nchi 200 zinazoshiriki kuongeza kasi ya utekelezaji wa hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi zinazochangia ongezeko la joto duniani.

Wito huo unafuatia tahadhari ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP), uliobainisha kuwa dunia inaelekea kuvuuka kiwango cha nyuzijoto 1.5 juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, ambacho ndicho kikomo kilichowekwa katika Makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 ili kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii